![]() |
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Valentino Mlowola |
Nchini
Tanzania katika Kijiji cha Ndami, tarafa ya Mwamashimba wilaya ya
Kwimba mkoani Mwanza watu wasiofahamika wamevunja nyumba na kumteka
mtoto mwenye ulemavu wa ngozi maarufu kama albino na kutoweka naye.
Watu
hao walivamia nyumba ya wazazi wa mtoto Pendo Emmanuel, mwenye ulemavu
wa ngozi wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye gizani baada ya
kuwazidi nguvu wazazi wake.
Emmanuel Shilinde mzazi wa mtoto huyo
ameieleza polisi kuwa majira ya saa nne usiku watu wawili waliuvunja
mlango wa nyumba yake kwa jiwe wakamchukua mtoto kwa nguvu kisha
wakakimbilia gizani kwa pikipiki.
Kamishina msaidizi mwandamizi wa
polisi mkoani mwanza Valentino Mlowola , ameitaarifu BBC kuwa leo ni
siku ya tatu na polisi bado ina matumaini ya kumpata akiwa hai motto
huyo, kwa kuwa bado hawajaupata mwili wake akiwa amepoteza uhai. Msako
unaendelea na tayari kuna watu watano wanazuiliwa na polisi ili kusaidia
kufahamu mtoto huyo yuko wapi.
Takwimu za kuanzia mwaka 2006
zinaonyesha kuwa Albino 74 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika
kifo, na kati yao 11 wamepata ulemavu mwingine wa kudumu.
Chapisha Maoni