SERIKALI imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua hatua stahiki katika shauri la kesi ya jinai namba 100 ya Jamhuri dhidi ya Isaac Emily aliyeadhibiwa kulipa faini kwa kumtukana Rais John Magufuli mtandaoni.


Hayo yamesemwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe wakati akitoa kauli ya serikali baada ya mwongozo ulioombwa na wabunge wa CCM, Juma Nkamia wa Jimbo la Chemba na Livingstone Lusinde wa Mtera, baada ya hukumu hiyo kutolewa hivi karibuni. Hata hivyo, hatua stahiki hizo hazikuelezwa.


Alisema nia ya maagizo hayo kwa DPP ni kulinda dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa haki jinai ambayo hutaka mhukumiwa kujutia kosa lake na wengine kujifunza kutoka kwake.


Katika maelezo yake, Waziri Mwakyembe alisema kwa hali ilivyo katika shauri hilo, dhana na dhamira ya adhabu haikuweza kufikiwa kwa mwenendo wa kuingiza siasa katika utekelezaji wa hukumu.

Alisema serikali imejiridhisha na kilichotokea katika shauri hilo na kauli za wabunge walioomba mwongozo kwamba masharti ya adhabu yalikuwa mepesi mno usiolingana na shauri lenyewe.


Alisema aliyehukumiwa analifanyia siasa suala hilo na kuigeuza adhabu rafiki aliyopewa kuwa burudani ya kisiasa katika mitandao ya kijamii.


“Mheshimiwa spika, nimejiridhisha na kilichotokea. Madhara ya mwelekeo huu mpya katika haki jinai, ni kuchochea vitendo zaidi vya ukaidi kwa mamlaka za nchi na hivyo kujenga msingi wa vurugu. Hili halikubaliki katika utawala wa sheria. Mdharau mwiba mguu huota tende,” alisema..



Alisema kosa kama hilo lilitokea Kenya mwaka jana ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini humo, Alan Okengo (25) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya dola 2,000 (Sh milioni 3.2) kwa kumtukana rais wa nchi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema pamoja na umri wake na uwezo wake mdogo wa kulipa faini, adhabu ilibaki palepale ili mkosaji ajutie kosa lake asije akarudia na jamii ijisikie salama.


Alisema pamoja na kutokuingilia mhimili wa mahakama na taratibu zake kitendo cha kuwapo kwa adhabu ambayo haijutiwi inakiuka dhana na dhamira ya adhabu.

Alisema kwa shauri la Emily, pamoja na kutiwa hatiani wakili wake aliomba mtuhumiwa alipe faini kwa kuwa hakusumbua mahakama na pia ni kosa lake la kwanza na ana familia.


Alisema wakati hakimu anamuuliza wakili wa serikali aliiachia mahakama kutoa maamuzi ambayo ilimpatia wakili wa utetezi maombi yake.


Mwakyembe alisema pamoja na maagizo ya serikali kwa DPP amewakumbusha waendesha mashitaka nchini kuwa macho na waweke mbele weledi na maslahi mapana ya taifa na kamwe wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika jamii.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Karibu tena..wasiliana nasi kwa simu namba 0758059936

Chapisha Maoni

 
Top