Marekani yataka Iran ishiriki vita dhidi ya Dola la Kiislamu
Marekani inakiri kuwa hata adui mkubwa, Iran, ana wajibu mkubwa kwenye
kulishinda kundi linalojiita "Dola la Kiislamu" ambalo limeshachukuwa
eneo kubwa la mataifa ya Syria na Iraq.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akizungumza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza kwenye kikao cha mawaziri wa nje wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa jijini New York, Kerry alisema katika juhudi za pamoja za
kimataifa dhidi ya kitisho cha kundi hilo, "takribani kila nchi ina
jukumu la kutekeleza, ikiwemo Iran."Wiki hii, Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alisema alikuwa amelikataa ombi la Marekani la kushirikiana nayo kwenye uwanja wa mapambano.
Ingawa maafisa wa Marekani hawajathibitisha wala kukanusha kutuma ombi hilo, lakini kimsingi wamekuwa hawaichukulii Iran kuwa sehemu ya muungano wanaouunda kupambana na Dola la Kiislamu.
Wiki iliyopita, mwanadiplomasia mmoja wa ngazi za juu wa Marekani alisema lisingelikuwa jambo muafaka kuialika Iran kwenye mikutano inayojaribu kujenga muungano huo wa kimataifa kutokana na "kujihusisha kwa serikali ya Iran nchini Syria na kwengineko."
Kwa upande mwengine, Iran inaziunga mkono serikali za Iraq na Syria katika vita vyao dhidi ya kundi hilo la Dola la Kiislamu.
Chapisha Maoni